Boya
Boya ni kifaa kinachowekwa katika maji ya bahari, ziwa au mto kwa makusudi mbalimbali.
Boya ama ni gimba lenye utupu ndani yake ili liweze kuelea kwenye maji, ama ni gimba linalotengenezwa kwa mata isiyozama kama plastiki au ubao mwepesi.
Kazi za boya mara nyingi ni kuwa alama ya njia kwenye maji; maboya yanaweza kudokeza mpaka ambapo boti au meli haitakiwi kupita tena, au mwisho wa eneo linaloruhusiwa kwa watu wanaoogelea.
Boya linalohitaji kukaa mahali pamoja hufungwa kwenye tako la bahari; kwa kawaida huwa na mnyororo uliofungwa kwenye jiwe kubwa au tofali la saruji inayozamishwa mahali panapotakiwa.
Bandarini kuna maboya makubwa yanayodokeza mahali pa kutia nanga. Boti dogo linaweza kufungwa moja kwa moja kwenye boya bila kutia nanga.
Maboya yanayoonyesha njia za maji (sehemu ambako kina cha maji yanatosha kwa meli) mara nyingi huwa na taa zinazohitaji huduma ya kubadilisha betri zake.
Maboya ya pekee huwa na vifaa vya upimaji ambavyo vinaweza kutumiwa kama kituo cha metorolojia; vingine hupima hali ya bahari vikielea bila kufungwa na kutuma data kwa njia ya redio.
Boyaokozi si boya halisi, bali kifaa cha kujiokoa wakati boti, meli au feri inazama na watu wanahitaji msaada wa kutozama.
Makala hii kuhusu mambo ya teknolojia bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu mada hiyo kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |